Saturday, May 23, 2015

PANYA WALA BATI

PANYA WALA BATI

(Nimetunga ushairi huu kwa heshima ya marehemu Omar Babu Marjan alituacha wiki jana_Mungu ailaze roho yake mahali pema peponi)

Malenga nimeshaketi,nimekabidhiwa cheti
Naiongoza kamati,inayotoa ripoti
Nimeshaikunja shati,tayari kula kaimati
Hawa panya wala bati,wanitia hatihati



Jombi kapewa kontrakti,na kukatiwa tikiti
Akanunua simiti,na vile vile mabati
Tulidhani kismati,tukamwachia penalti
Hawa panya wala bati,wanitia hatihati



Alijenga kiunati,akafuata masharti
Akaezeka makuti,hayakutosha mabati
Akasema panya eti,wameguguna mabati
Hawa panya wala bati,wanitia hatihati


Twapitia vyake vyeti,tukaona yuko fiti
Alifanya mikakati,‘katufyonza kama titi
‘kachukua wake switi,‘kaabiri kubwa jeti
Hawa panya wala bati,wanitia hatihati


Aliangika soketi,zenye urefu wa goti
Katumia ghushi nati,koromeo kudhibiti
Tumepata kubwa soti,maelezo hatupati
Hawa panya wala bati,wanitia hatihati


Alivyotumia senti,akiulizwa ‘hanyiti‘
Ananuna kama nyati,na faili za risiti
Tushapata idhibati,yaliko yote mabati
Hawa panya wala bati,wanitia hatihati


Waliguguna mabati,iliyeyuka simiti?
Mwenzangu huna bahati,utaozea Kamiti
Bora ule ratirati,isilipuke baruti
Namaliza utafiti,nimefikia tamati
Navua yangu kaputi,‘shaisha wangu wakati
Nimeshalenga manati,na kupiga kibiriti
Hawa panya wala bati,wanitia hatihati


UTUNZI WA ‪‎Jicho‬ La Pembeni Malenga Wa Nchi Kavu©2015

No comments:

Post a Comment